Waziri wa Maji, Prof Jumanne Maghembe akizungumza na waandishi wa habari |
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe ameshangazwa na utitiri wa watu wanaotaka kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2015, akisema nafasi hiyo ya juu nchini haifanani na mashindano ya urembo ambayo mtu yeyote anaweza kujaribu.
Mbunge huyo wa Mwanga alisema watu hao
wanaojitokeza kuwania urais hawaelezi wanataka kulifanyia nini Taifa na
akashauri wasioweza kueleza hoja zao wasichaguliwe kushika nafasi hiyo.
“Urais unahitaji kuwa na sifa, dira na ajenda kwa
Taifa,” alisema Profesa Maghembe wakati wa mahojiano maalumu na gazeti
hili mjini hapa.
Kauli ya Profesa Maghembe imekuja wakati Taifa
likijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, 2015, huku chama
chake, CCM kikikabiliwa na kazi ngumu ya kumpata mrithi wa Rais Jakaya
Kikwete ambaye anamaliza muda wake.
Hali kama hiyo iliikumba CCM wakati wa uchaguzi wa
kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 wakati takriban watu 20 walipojitokeza
kutaka kuingia Ikulu na baadaye mwaka 2005 wakati wa uchaguzi
uliomuweka madarakani Rais Kikwete.
Ndani ya CCM, mjadala huo sasa umekumbwa na hoja
ya umri baada ya makada vijana kujitokeza kutangaza nia ya kumrithi Rais
Kikwete kupambana na wanasiasa wakongwe, baadhi wakiwa ni wale
waliojiandaa kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Profesa Maghembe alipuuza mjadala huo
wa umri wa mtu kugombea urais akisema kuwa hauna msingi na kwamba sifa
kuu ya mgombea urais ni ajenda ya kuliletea Taifa maendeleo endelevu.
“Umri hauwezi kuleta tofauti katika uongozi wa
nchi. Ni kama kusema jiwe liwe rais,” alisema mwanasiasa huyo mkongwe,
ambaye amefanya kazi wizara tofauti tangu Januari 2006 aliposhika
uwaziri kwa mara ya kwanza.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka mgombea urais awe na umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea.
“Hivyo haisemi kuwa ukishakuwa na miaka 70 huwezi
kuwa rais ama haisemi ukiwa na miaka 40 unafaa zaidi kuwa rais.
Inategemea huyo mtu anayegombea anataka kuwafanyia nini Watanzania,”
alisema.
Waziri huyo wa saba tangu Wizara ya Maji
ianzishwe, alisema kugombea urais kunategemea ajenda aliyonayo mtu na
hata watu wanapokwenda kumchagua, lazima waangalie ana ajenda gani.
“Ikulu si mahali pa kukimbilia, mimi hata sijui wanakimbilia nini kwa
sababu lazima mtu uwe na ajenda. Na kama mnasikia mtu anasema mimi
nataka kuwa tu rais, huyo hafai kabisa,” alisema.
“Lazima mtu anayetaka kuwa rais atueleze uchumi
sasa unakua kwa asilimia saba na umekuwa hivi kwa karibu miaka 10 lakini
ni jambo linalofanya umaskini uwe mkali kabisa na usiishe ni kutokana
na shughuli inayofanywa na watu wengi ya kilimo, kuwapatia kipato haikui
kama sekta nyingine.
Chanzo; MWANANCHI COMMUNICATIONS
Chanzo; MWANANCHI COMMUNICATIONS
0 comments:
Post a Comment