Imeelezwa kuwa maambukizi ya Virusi vya
Ukimwi (VVU), yanaweza kuongezeka nchini hasa kwa vijana kutokana na
kubainika kupungua kwa kasi ya matumizi ya mipira (kondomu).
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Florens Turuka katika mkutano wa sita wa
kutathmini maambukizi ya VVU nchini.
Dk Turuka alisema maambukizi mapya yameendelea kuwapo kwa sababu vijana hawatumii kondomu kujikinga.
“Matumizi ya kondomu katika jamii
yamepungua na kuwafanya watu wengi hasa vijana kupata maambukizi na
zaidi ni kutokana na mwamko mdogo kuhusu umuhimu wa kondomu kama kinga
ya Ukimwi,” alisema.
Alisema utafiti uliofanyika mwaka jana
ulionyesha kuwa asilimia 50 ya waliojitokeza kupima VVU na kupata
ushauri, walikiri kutotumia kondomu. Hata hivyo, Dk Turuka alisema
katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, maambukizi mapya yalipungua
kutoka watu 180,000 hadi 72,000 kwa mwaka.
Alisema licha ya kuwapo mafanikio hayo,
kiwango cha matumizi ya kondomu kimeshuka na kuhatarisha maisha ya
vijana wenye umri kati ya miaka 15 – 39.
Alisema mwaka ujao wa fedha, Serikali
itaanzisha mfuko maalumu wa kukusanya fedha kwa ajili ya kununulia dawa
za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARV).
Alisema zaidi ya nusu ya wagonjwa walioathirika wanahitaji dawa hizo.
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya
Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Fatma Mrisho alisema wanafanya jitihada
kuhakikisha wanapunguza maambukizi mapya hadi kufikia sifuri ifikapo
mwaka 2020.
Aliitaja baadhi ya mikoa yenye idadi kubwa ya maambukizi mapya kuwa ni Njombe, Shinyanga, Mbeya, Dar es Salaam na Ruvuma.
“Katika miaka miwili ijayo, tutaelekeza
nguvu zetu kwenye mambo yanayochangia kuongezeka kwa maambukizi mapya,
ikiwamo maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kukabiliana na
uhaba wa dawa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment