NA FONIA BUNDALA
Rais Obama wa Marekani na Putin wa Urusi walikutana Jumanne mjini
Beijing, kandoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikisho wa Kiuchumi ya
nchi za Asia na Pasifik - APEC . Kuzungumzia masuala ya Iran ,Syria na
Ukraine.
Uhusiano baina ya Marekani na Urusi uko katika kiwango cha chini kabisa
tangu kumalizika enzi ya vita baridi, huku Urusi ikiekewa vikwazo
vinavyoongozwa na Marekani kutokana na hatua yake ya kulitwaa eneo la
Ukraine la Crimea mwaka huu, pamoja na mchango wake katika vita vya wale
wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine
.
Marais hao wawili hata hivyo walikutana kwa mazungumzo yasio rasmi kwa
karibu dakika 15 hadi 20 wakati wa mkutano huo wa kilele wa APEC
kaskazini mwa mji mkuu wa China.
Nchi zote mbili-Marekani na Urusi- zinahusika katika mazungumzo kati ya
madola matano yenye nguvu pamoja na Ujerumani kwa upande mmoja na Iran
upande wa pili , kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran
. Lakini
kuhusiana na Syria Urusi ni mshirika wa karibu wa utawala wa Rais Bashar
al-Assad, na imemuunga mkono katika kipindi chote cha vuguvugu
lililoanza Machi 2011 dhidi ya utawala wake.
Tafauti baina ya Marekani na Urusi juu ya Ukraine
Lakini tafauti kubwa za mtazamo hivi sasa kati ya Marekani na Urusi ni
kuhusiana na Ukraine. Katikati ya mwezi Oktoba Putin alimshutumu Obama
kuwa anajenga tabia ya uhasama dhidi ya Urusi, wakati Obama alikosoa
kile alichokiita "uchokozi," wa Urusi dhidi ya Ulaya wakati
alipolihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
Hapo mapema naibu waziri wa Marekani anayehusika na usalama wa taifa Ben
Rhodes, aliwaambia waandishi habari mjini Beijing kwamba " tunaendelea
kusumbuliwa na harakati za Urusi katika Ukraine na ikiwa zitaendelea ni
sababu moja ya kuitenga."
Wakati mkutano wa kilele wa APEC mjini Beijing, umemalizika Obama na
Putin pia watahudhuria mkutano wa kilele mataifa 20 yenye nguvu
kiuchumi, kundi linalojulikana kama G20. Mkutano huo utafanyika mjini
Brisbane-Australia tarehe 15 na 16 Novemba. Hata hivyo haikufahamika
ikiwa huko nako watakutana tena kwa mazungumzo mengine kandoni mwa
mkutano huo.
Ikulu ya Marekani imeshasema kwamba sawa na ilivyokuwa mjini Beijing ,
hakuna mpango wowote wa Obama kukutana na Putin kwa mazungumzo rasmi.
CHANZO DW
0 comments:
Post a Comment