Mtoto Hassan Masasi, aliyetoroka nyumbani kwao Moshi, Kibosho-Umbwe, mkoani Kilimanjaro.
Mtoto Hassan Masasi (pichani), aliyetoroka nyumbani kwao Moshi, Kibosho-Umbwe, mkoani Kilimanjaro, ameonekana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza jana katika ofisi za gazeti hili zilizoko Mikocheni jijini Dar es Salaam, mtoto huyo mwenye umri wa miaka saba, alisema ni mwanafunzi wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Kindi Juu, iliyopo Moshi, Kibosho- Umbwe.
Alimtaja mama yake mzazi kuwa ni Pendo Athanas, mkazi wa eneo hilo na baba yake anaitwa asasi anayeishi Bukoba.
Hata hivyo, alisema wakati anaondoka nyumbani kwao, hakugombezwa na mtu yeyote wala kufanyiwa kitendo chochote kibaya isipokuwa aliamua mwenyewe kupanda basi la kampuni ya Buffalo bila kulipa nauli lakini alikuwa hajui anakokwenda.
Alisema alipofika Dar es Salaam, alipanda gari la kwanza akashuka na kisha kupanda lingine ambalo lilimfikisha eneo aliloliita ‘Bom-bom’ ambako alikuwa anatunzwa na msamaria mwema ambaye hamjui jina lake.
Mlinzi katika kampuni ya pikipiki iliyopo Mwenge mkabala na Kanisa la Efatha, jijini Dar es Salaam, Dotto Mkonda, alisema alimkuta mtoto huyo eneo la Mlalakuwa jana.
Dotto aliyemfikisha mtoto huyo katika ofisi za gazeti hili, alisema alimkuta katika kichochoro huku akiwa amechoka kiasi cha kuzungumza kwa taabu.
Alisema baada ya kumpa chakula, alimpeleka kituo kidogo cha polisi cha Mwenge ambako alifunguliwa jalada namba MWG/RB/1743/2014.
Amewataka watu wanayemfahamu mtoto huyo kwenda katika Kituo cha Polisi Mwenge ama cha karibĂș au kupiga simu namba 0716 87 86 41.